- Wakunwa na hatua dhidi ya vigogo Escrow
NA MUSSA YUSUPH
NCHI na mashirika wahisani wameanza mchakato wa kutoa fedha za msaada wa bajeti walizozizuia, kutokana na sakata la uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, baada ya kuridhika na hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.
Fedha zitakazotolewa ni sh. bilioni 922, ambazo ni sehemu ya asilimia tano zitakazotumika kusaidia bajeti, ambapo kabla ya kuzuliwa, asilimia 20 ya fedha hizo, zilikuwa zimekwishatolewa kwa serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam,jana, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya Salum, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya mashirika na nchi zinazochangia bajeti kujadiliana na serikali kwa kina, kuhusu hatua zilizochukuliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Alizitaja taasisi zingine zilizoshiriki majadiliano hayo kuwa ni, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na Bunge huku wafadhili hao wakiahidi baada ya wiki moja kutoa sh. bilioni 70 kama hatua ya awali.
Alisema wafadhili wengine, ambao ni Umoja wa Ulaya pamoja na Benki ya Dunia, wameanza kufanya vikao vya bodi ili kupitisha msaada wa sh. bilioni 300.
Akizungumzia kuhusu kutengwa kwa asilimia 20 kama fedha za maendeleo na kusababisha kuchelewa kukamilika kwa miradi hiyo kutokana na uchache wa fedha zinazotengwa, alisema hakuna ukweli juu ya jambo hilo.
Saada alisema asilimia 65 ya fedha zinazotengwa na serikali kwenye bajeti, hutumika kwenye shughuli za maendeleo huku kiasi kikubwa cha fedha hizo ni za mapato ya ndani.
Aliongeza kuwa kucheleweshwa kwa miradi kunatokana na baadhi ya watendaji wa serikali kutotoa ripoti ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa awamu husika, hivyo serikali haiwezi kutoa fedha pasipo kuridhika namna zilivyotumika awali.
“Serikali haiwezi ikatoa fedha pasipo kujua matumizi ya fedha zilizopelekwa awali kwenye mradi husika, hivyo lazima tufahamu namna uwasilishwaji wa ripoti ya mradi inavyocheleweshwa ndivyo fedha huchelewa kutolewa,” alisema.
Alisisitiza kuwa mradi ukitekelezwa pasipo kufuata utaratibu, ni vigumu kwa serikali kutoa fedha.
Kwa upande wake, Balozi wa Finland nchini, Sinikka Antila, alisema wataendelea kushirikiana na serikali kupambana na vitendo vya ubadhirifu pamoja na kulipongeza Bunge kwa kuendesha majadala wa sakata la Escrow kwa uwazi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru