Tuesday, 3 March 2015

TMA: Ukame kuishambulia nchi masika
NA WILLIAM SHECHAMBO
KIWANGO cha mvua katika msimu wa mwaka huu wa masika ni kidogo kwenye maeneo mengi ya nchi hali inayoweza kusababisha ukame endapo Watanzania hawatazitumia kwa busara mvua chache zinazotarajiwa kunyesha nchini.
Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), juu ya mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa, ulisema licha ya maeneo mengi ya nchi kutarajia mvua za wastani, maeneo mengine mvua zitakuwa kubwa.
Baadhi ya maeneo hayo ni kanda ya Ziwa Viktoria, mikoa ya Kagera, Simiyu na mikoa ya kusini mwa nchi ukiwemo Lindi, Ruvuma, Mtwara na Mashariki mwa mkoa wa Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisi za TMA, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa wa Mamlaka hiyo, Dk. Agnes Kijazi, alisema kwa mwaka huu masika inakuja na mvua chache kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Dk. Agnes alisema pia licha ya mabadiliko hayo, ambayo wengi walitarajia unafuu wa hali ya hewa katika kipindi hiki ambacho maeneo mengi likiwemo jiji la Dar es Salaam joto limekuwa juu, kuna uwezekano wa kuwepo vipindi vichache vya mvua kubwa kwenye baadhi ya maeneo.
Alisema katika utabiri wa msimu wa vuli walioutoa Oktoba, mwaka jana, walisema maeneo mengi ya nchi yangekuwa na mvua za wastani na juu ya wastani, huku wakiutaja mkoa wa Ruvuma pekee kuwa na mvua ya chini ya wastani.
Pia katika utabiri huo wa vuli, alisema walitabiri mvua za juu ya wastani kwenye maeneo ya kanda ya Ziwa Viktoria hali iliyotokea kwa usahihi, lakini makadirio ya utabiri yakawa chini ya wastani wao kwenye mikoa ya pwani ya bahari ya Hindi kutokana na mabadiliko ya mfumo wa bahari.
Mkurugenzi huyo alisema kwa mikoa ya kaskazini mashariki, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro pamoja na ile ya Kanda ya Ziwa, mvua zinatarajiwa kuanza wiki yoyote mwezi huu kwenye baadhi ya maeneo.
Pia alisema kwenye mikoa ya Maghariki mwa nchi, Kigoma, Katavi, Tabora na Rukwa, ambayo hupata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, mvua zilianza kunyesha Novemba mwaka jana na zinatajiwa kukata wiki ya pili na ya tatu ya Aprili mwaka huu.
Kutokana na Utabiri huo, ambao Dk. Agnes alisema matokeo yake yamesababishwa na mabadiliko kadhaa katika mifumo ya hewa na ongezeko la joto katika bahari ya Hindi na Atlantiki, wadau kadhaa walisema ni msimu wa tahadhari kubwa.
Jubilathe Bernard, Ofisa kutoka idara ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, mlipuko kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, aliosema Wananchi wanapaswa kuzingatia usafi kutokana na uwezekano wa kutokea magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji.
Pia alisema kwenye maeneo yanayotarajiwa kuwa na mvua nyingi, wahusikia wanapaswa kuchukua tahadhari kiafya.
Kwa upande wao, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Karim Mtambo, alisema wananchi wanatakiwa watumie chakula walichonacho kwa busara, wasiuze chakula na pia walime mazao yanayowahi kukomaa na  yale yanayostahimili ukame ikiwemo Mihogo na Mtama.

1 comments:

 1. Tunaomba TMA mkae na Wizara ya Kilimo ili kutoa ushauri unaomsaidia mkulima.
  1. Mvua zinaanza lini katika maeneo hayo
  2. Wanashaurika kulima kuanzia lini na mazao gani
  3. Kila maafisa ughani wapewe barua na mkurugenzi ili wajue kipi cha kumsaidia mkulima. Hii namaanisha elimu waliyonayo haiendani na haya mabadiliko hivyo wakipewa hiyo inakuwa kama refreshier course.
  4. otherwise hizi taarifa hazina msaada kwa ngazi ya mkulima

  ReplyDelete