Thursday, 12 March 2015

Zitto aitunishia misuli CHADEMA



  • Ofisi ya Bunge, NEC zaikana CHADEMA
  • Dk. Kitilla: Upinzani unaua demokrasia

NA WAANDISHI WETU
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema hatambui kufukuzwa uanachama wala ubunge wake na kwamba, ataendelea na majukumu ya kuwatumikia wananchi wake kama kawaida.

Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Ofisi ya Bunge, zimesema hazijapokea barua wala taarifa kutoka CHADEMA za kumvua uanachama mbunge huyo.
Aidha, baadhi ya wanasiasa akiwemo Profesa Kitila Mkumbo, wameponda uamuzi unaofanywa na vyama vya upinzani kuwafukuza na kuwavua madaraka wanachama wake kuwa, ni vitendo vya ukandamizaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Zitto alisema ataendelea kufanyakazi zake za ubunge npaka atakapopokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Alisema kama amefukuzwa uanachama wa CHADEMA, zipo taratibu zinazotakiwa kufuatwa, ikiwemo Ofisi ya Spika kuandikiwa barua na kuridhia maamuzi hayo.
“Kama nimefukuzwa ilitakiwa Ofisi ya Spika wa Bunge ipewe taarifa rasmi na iandike barua ya kuridhia uamuzi huo, lakini hadi sasa sijapewa taarifa yoyote, hivyo bado ni mbunge halali.
“Mpaka muda huu sifahamu chochote kinachoendelea na habari za kufukuzwa kwangu nimezipata kupitia kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Zitto.
Aliongeza:  “Kama mnavyoniona, naendelea kutekeleza majukumu yangu ya kuwatumikia wananchi kama nilivyoahidi, kesho na kesho kutwa nitaendelea kuongoza vikao vya kamati yangu kama ratiba inavyoonyesha.”
Zitto alisema kazi yake ni tofauti na wabunge wengine na kwamba, ni mtu wa kazi na si wakujibizana.
Aidha, alisema haoni haja ya kulumbana na uongozi wa CHADEMA kwani, kazi yake ni kuwatumikia wananchi na si malumbano.
“Niko tofauti na wabunge wengine, mimi ni mtu wa kazi sio wa kulumbana kama wanavyofanya wengine. Hizi zote ni changamoto tu za kisiasa, nakuzwa na kukomazwa zaidi kisiasa, siwezi kulinganishwa na mbunge yeyote nchini, kila mtu anafahamu hilo,” alisisitiza Zitto.
Alisema kabla ya kuanza vikao vya Bunge, anatarajia kwenda jimboni kutekekeza baadhi ya mambo kama alivyowaahidi wananchi wake.
Jaji Lubuva aongea
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva, alisema ofisi yake haijapata taarifa yoyote kutoka CHADEMA, Ofisi ya Spika ama Ofisi ya Mrajisi wa Mahakama Kuu, ya kuvuliwa uanachama Zitto.
Alisema taarifa hizo wanazisikia na kuzisoma kwenye vyombo vya habari, lakini hazijawafikia rasmi.
“Hata kama amefukuzwa, ofisi yangu haijapewa taarifa na unajua hii kesi ilihukumiwa jana (juzi), hivyo ana haki ya kukata rufani iwapo hakuridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama,” alisema.
Alisema iwapo maneno yanayozungumzwa ni sahihi, bado hakutakuwa na uchaguzi mdogo kwa sasa kwa kuwa sheria hairuhusu.
Ofisi ya Bunge
Ofisi ya Bunge jana ilisema haijapokea taarifa yoyote kutoka CHADEMA inayoeleza kuwa Zitto amefukuzwa uanachama.
Mmoja wa maofisa wa Bunge, ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini kwa sababu si msemaji wa Bunge, alisema bado wanamtambua Zitto kama mbunge wa Kigoma Kaskazini.
“Hadi muda huu hatujapata taarifa yoyote kutoka CHADEMA, hivyo tunamtambua Zitto kama mbunge halali na ataendelea na shughuli zote za kibunge,” alisema.
Ukandamizaji demokrasia
Mtaalamu wa Elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Kitilia Mkumbo, alisema kitendo kilichofanywa na CHADEMA ni aibu na kwamba, kinapora mamlaka ya wananchi ambao ndio wamemchagua mbunge.
Dk. Kitilla, ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA kabla ya kutimuliwa mapema mwaka jana, alisema ndani ya chama hicho kuna matatizo makubwa na kuhoji uhalali wa Tundu Lissu kumfukuza mtu uanachama bila ya Baraza Kuu.
“Kilichotokea jana (juzi) ni dhahiri kwamba CHADEMA hawana jipya na wananchi wanapaswa wajiulize ni sahihi kuendelea kuvipa dola vyama ambavyo vinaendeshwa kifalme,” alihoji.
ILIVYOKUWA
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, juzi, ilitupilia mbali kesi ya msingi iliyokuwa imefunguliwa na Zitto dhidi ya chama hicho.
Kutokana na kutupiliwa mbali kesi hiyo, uongozi wa CHADEMA, ulitangaza kumtimua uanachama na kumvua nyadhifa zake zote za kichama.
Uamuzi wa mahakama ulitolewa na Jaji Richard Mziray, baada ya kukubaliana na moja ya mapingamizi ya awali yaliyowasilishwa na mawakili wa CHADEMA, kupinga kesi hiyo.
Zitto alifungua kesi hiyo namba moja ya mwaka jana, dhidi ya bodi ya wadhamini ya chama hicho na Katibu Mkuu wa CHADEMA.
Katika shauri hilo, alikuwa anaiomba Mahakama iamuru Kamati Kuu ya CHADEMA na chombo chochote cha chama hicho, kutojadili na kuchukua uamuzi kuhusu uanachama wake hadi rufani yake itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi na baraza kuu la chama hicho.
Pia alikuwa anaiomba mahakama imwamuru katibu mkuu huyo, ampatie mwenendo wa kikao cha Novemba 22, mwaka jana, cha baraza kuu ambacho kilifikia uamuzi wa kumvua nyadhifa zake zote za kichama.
Baada ya mahakama kutoa uamuzi huo, CHADEMA, kupitia mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, alitangaza kumfukuza uanachama Zitto na kusema kuwa alikiuka utaratibu kwa kuwa hakupaswa kufungua Mahakama Kuu ya Tanzania bali Mahakama ya Mkazi au Masijala ya Wilaya ya Mahakama Kuu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru