Monday, 16 March 2015

‘Vijana changamkieni mkutano wa jukwaa’NA MWANDISHI WETU
VIJANA wametakiwa kujitokeza kushiriki Mkutano wa Jukwaa la Tatu la Kimataifa la Viongozi Vijana wa Afrika na China, linaloandaliwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Aidha, jukwaa hilo linalohusu kudumisha urafiki, ushirikiano na maendeleo, baina ya vijana wa Afrika na China kiuchumi, kisiasa na kijamii, linatarajiwa kufanyika jijini Arusha, kuanzia Machi 27 hadi 31, mwaka huu.
Sixtus Mapunda
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, alisema jasna jijini Dar es Salaam kuwa mkutano huo utahudhuriwa na vyama vya siasa 57 kutoka  nchi 43 za Afrika.
Vile vile, alisema kutakuwa na vijana wafanyabiashara 32 kutoka nchi mbalimbali za Afrika watakaoungana na wenzao 70 toka Tanzania na wengine 50 wa China kujadili fursa zilizopo na jinsi ya kuzifikia ili vijana wa Afrika waweze kujiletea maendeleo.

“Ni wasaa mzuri ambao vijana wa Tanzania walikuwa wakiusubiri, hivyo ni vyema wakajitokeza kwa wingi ili kuona fursa zilizopo na kuzitumia kujiletea maendeleo,” alisema.

Mapunda alisema mada zitakazojadiliwa katika jukwaa hilo ni maendeleo na uhusiano kati ya Afrika na China, ushiriki na uhusiano wa vijana kimaendeleo na wajibu wa asasi za kiraia wa kukuza uhusiano na maendeleo kati ya Afrika na China.
Alisema jukwaa hilo ni la tatu ambapo la kwanza lilifanyika mwaka 2011, mjini Windhoek, Namibia, likifuatiwa na lile la Beijing, China mwaka 2012.
Alitaja viongozi watakaohudhuria jukwaa hilo kuwa ni Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China na Tanzania  na mawaziri wa hapa nchini wa Viwanda na Biashara na Nishati na Madini, huku Rais Jakaya Kikwete akiwa mgeni rasmi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru