Friday 13 March 2015

Slaa abanwa kwa saa tano



  • Ni unyama aliofanyiwa Kagenzi na madai ya kutaka kudhuriwa

NA MWANDISHI WETU
SAKATA la kushambuliwa kwa aliyekuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, Khaild Kangezi, limechukua sura mpya baada ya kiongozi huyo kufika katika kituo kikuu cha polisi na kuandika maelezo kwa takriban saa tano.
Hivi karibuni,  Dk. Slaa kupitia kwa mmoja wa viongozi wa CHADEMA, Mabere Marando, alidai kuwepo kwa mpango wa kumdhuru, ambao unaratibiwa na maofisa usalama kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa CCM.

Mpango huo ulidaiwa kuwa ungetekelezwa kupitia kwa Kangezi, ambaye baadaye aliteswa na kushambuliwa na wafuasi wa chama hicho, ikiwa ni mkakati wa kumlazimisha kukiri.
Tayari Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amewataka Watanzania kupuuza uzushi wa Dk. Slaa na kueleza kuwa, amekuwa mtu wa kuibua tuhuma za uzushi na uongo kila kukicha.
Juzi, Kangezi alikanusha madai ya kukiri kutaka kumdhuru Dk. Slaa na kueleza kuwa, alishinikizwa kukiri suala hilo na baadhi ya wanachama wa CHADEMA, ambao walimpa vitisho.
Dk. Slaa alifika kituoni hapo jana  saa 4.00 asubuhi, akiwa katika gari namba T 834 BJG aina ya Toyota Land Cruiser, akiwa na mawakili wa chama hicho, John Mallya na Nyaronyo Kicheere.
Baada ya kufika kituoni hapo, Dk. Slaa alikwenda kutoa maelezo yake na kumaliza kuyatoa saa 9:37 alasiri.
Baadaye alitoka na kuwaeleza waandishi wa habari kuwa, muda wote alikuwa akiandika maelezo kuhusiana na sakata hilo.
Alisema aliandika kwa mkono wake maelezo ya kurasa tisa na alipewa haki zote na hakukuwa na mazingira ya vitisho.
Hata hivyo, hakuwa tayari kueleza alichoandika kwenye kurasa hizo kwa madai bado suala hilo linaendelea kuchunguzwa.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alisema kuna vijana watatu wa CHADEMA, wanaendelea kushikiliwa kutokana na Kangezi kufungua kesi ya kushambuliwa.

NAPE: Babu ni mzushi
Juzi, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Nape alisema madai ya Dk. Slaa dhidi ya CCM na serikali ni propaganda za kitoto na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ili kujenga taifa.
“Namshauri baba yangu (Dk. Slaa) kwa umri wake, wenzake wakifikisha umri wa uzee ni wakati mzuri kumrejea Mwenyezi Mungu, badala ya kutunga taarifa za uongo na uzushi kila kukicha,” alisema.
Alisema CCM na serikali vina majukumu makubwa ya kuwatumikia Watanzania na kamwe haina muda wa kupoteza.
Nape alisema tuhuma hizo ni za kipuuzi, lakini uongo huo usipojibiwa, unaweza kugeuzwa kuwa ajenda kutokana na CHADEMA kutokuwa na ajenda za maana na zenye tija kwa taifa.
Alisema Chama hicho kwa sasa kiko kwenye hali ngumu na kinapumulia mashine na kwamba ni lazima kipange mikakati ili kiweze kujinasua.  
Kangezi aweka mambo hadharani
Kwa upande wake, Kangezi alikana kuhusika na madai ya kutaka kumdhuru Dk. Slaa na kwamba, wakati wote alifanya kazi yake kwa nia ya kuwakomboa Watanzania.
‘’Sikununuliwa na CHADEMA bali nilifanya kazi kwa kujitolea kwa manufaa ya Watanzania,’’ alisema.
Alisema kitendo cha kudaiwa kuwa alipanga njama za kutaka kumuua Dk. Slaa, hazina ukweli na kuwa alishinikizwa na baadhi ya wanachama wa CHADEMA kumtaka kukiri kutokana na vitisho alivyokuwa akivipata.
‘’Niliamua kukiri kuhusika kutokana na vipigo nilivyokuwa nikivipata kwa baadhi ya wanachama wa chama hicho kutaka niseme kuwa nimefanya hivyo,’’ alisema.
Alimtaja mmoja wa watu hao kuwa ni Benson Mramba, ambaye alitoka nje na wenzake kutafuta usafiri na kupanga njama za kumuua.
Pia, alisema wanachama hao walimshinikiza kuwahusisha maofisa usalama kuwa wapo kwenye njama za kutaka kumdhuru Dk. Slaa, jambo ambalo halina ukweli.
Hata hivyo, alisema kamwe hatanyamaza kutokana na unyama na udhalilishaji aliofanyiwa na kwamba, atapambana kutafuta haki yake.
‘’Nilipigwa na kuvuliwa nguo zote na kubaki kama nilivyozaliwa huku nikipata kipigo kikali…inauma sana na sina sababu ya kukaa kimya katika hili,’’ alisema. 
Kangezi aliwataka wananchi kufanya uamuzi sahihi kuchagua viongozi, ambao watahakikisha amani inaendelea kuwepo nchini.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru