Wednesday, 11 March 2015

Mbivu, mbichi za Tibaijuka kesho


NA MARIAM MZIWANDA
HUKUMU ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kuhusiana na kupata mgawo wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, inatarajiwa kutolewa kesho.


Profesa Tibaijuka, tayari amehojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma juu ya tuhuma hizo, ambapo alikiri kupata mgawo huo, lakini akaeleza kuwa ulikuwa ni msaada. Anatuhumiwa kukiuka  Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma namba 12 (e) (1) ya mwaka 1995.
Mwanasheria wa Baraza hilo, Wema Winfred, alidai Profesa Tibaijuka, anakabiliwa na mashitaka matatu, ambayo ni kuomba fadhila za kiuchumi kinyume na sheria ya maadili kifungu namba 6, kupokea fadhila za kiuchumi kinyume na sheria hiyo na kuwa na mgogoro wa kimaslahi.
Anadaiwa kukiuka maadili ya umma kwa kuomba kuingiziwa fedha kiasi cha sh bilioni 1.6 kutoka katika Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, ambazo aliingiziwa kwenye akaunti namba 001200102640201 iliyopo Benki ya Mkombozi, Tawi la St. Joseph mjini Dar es Salaam.
Kutokana na hatua hiyo, Tibaijuka alidaiwa 
kutumia wadhifa wake kujinufaisha kifedha, hivyo baraza kueleza mwenendo wake kabla ya hatua zaidi za kisheria.
Mwanasheria wa Profesa Tibaijuka, Dk. Rugemaleza Nshara, alipinga  tuhuma hizo na  kudai mteja wake ameonewa katika shauri hilo 
Naye shahidi wa upande wa mlalamikaji,  Katibu Msaidizi Idara ya Uongozi wa Siasa wa Sekretarieti hiyo, Waziri Kipache (45), alisema 
Aprili 4, 2012, Profesa Tibaijuka aliomba fedha kwa mke wa mmiliki wa Kampuni ya VIP, James Rugemalila na maombi hayo yaliwasilishwa kwa barua.
Kipache alitoa maelezo yake mbele ya jopo la viongozi wa Baraza la Maadili na uthibitisho wa barua ya Profesa Tibaijuka ya kuomba fedha hizo.
“Kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma, hawaruhusiwi kuomba fedha kwa maslahi ya kiuchumi, hivyo basi Profesa Tibaijuka ametenda kosa ,” alisema Kipache.
Profesa Tibaijuka, alijitetea mbele ya baraza hilo na kulieleza alivyotumia fedha za mgawo wa Escrow, ikiwamo kutumia sh milioni 10 kwa ajili ya kununua mboga.
Alikiri kuomba fedha hizo, lakini si kwa maslahi yake binafsi, bali ni kwa ajili ya Taasisi ya Barbro Johannson Girls Trust.
Kutokana na madai hayo na utetezi wa waziri huyo wa zamani wa serikali ya awamu ya nne, hukumu yake inatarajiwa kutolewa kesho, baada ya awali wakili wake kuomba udhuru.
Jaji mstaafu Hamis Msumi, alikubali ombi hilo na baraza litaamua hukumu kuwa ya namna gani, kama iwe ya uamuzi wa ndani au hadharani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru