NA KHADIJA MUSSA
MWENYEKITI wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Dk. Stephen Bwana, amewataka watumishi wa umma kujiepusha na ushabiki wa siasa za mpito, badala yake wazingatie katiba, miiko na maadili ya utumishi wa umma.
Alisema kuna upungufu katika uzingatiaji wa maadili, hivyo aliwataka watumishi hao kubadilika na kutojihusisha na ushabiki wa siasa, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwani hakuna nchi duniani, ambayo watumishi wake hawazingatii maadili.
Pia aliahidi kushughulikia matatizo ya upungufu wa maadili kwa watumishi wa umma kwa sababu amekuwa akisikia na kusoma malalamiko mbalimbali ya watumishi wa umma kutozingatia miiko na maadili.
Dk. Bwana, ambaye ni jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, aliyasema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam, baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, kushika wadhifa huo ambapo aliahidi kushughulikia matatizo ya upungufu wa maadili.
Alisema matatizo yako pande zote kwa waajiri na waajiriwa, hivyo alizishauri pande zote kufuata maelekezo, ambayo kila mtumishi wa umma anapoajiriwa kuna mambo anaelekezwa.
Mwenyekiti huyo alisema atahakikisha wanatilia mkazo suala la watumishi wa umma kufanyakazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi, ambazo huelekezwa wanapoajiriwa, lakini baadhi yao hawazitekelezi.
Kuhusu suala la kuwepo kwa watumishi wengi kukaimu nafasi mbalimbali kwa muda mrefu, alisema watalishughulikia na kulitolea taarifa kwa kuwa sheria zipo na mtu haruhusiwi kukaimu nafasi yoyote kwa zaidi ya miezi sita.
Mbali na Dk. Bwana, Rais Kikwete pia aliwaapisha makamishna wa tume hiyo, ambao ni George Yambesi, aliyekuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Alhaj Yahaya Fadhili Mbila, Mgeni Mwalimu Ally, Adieu Nyondo, Salome Mollel na Evelyne Itanisa.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Evelyne alisema tume hiyo ina majukumu mazito ya kushughulikia watumishi wa umma ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa kuzingatia maadili.
Alisema jukumu lingine watakalolipa uzito ni kuhakikisha watu wanaajiriwa kwa kuzingatia uzoefu, taaluma na uwezo wa kiutendaji na si vinginevyo.
Sambamba na hayo, kamishna huyo alisema watafuatilia kwa makini suala la nidhamu kwa waajiri na waajiriwa, lengo likiwa kuimarisha heshima kwa watumishi wote kwa sababu hakuna aliye juu ya sheria.
Evelyne alisema suala lingine litakalotiliwa mkazo ni kuhusu mfumo wa upimaji wa watumishi katika utekelezaji wa majukumu yao na mikataba ya kazi, kwa sababu kuna baadhi ya taasisi hawazingatii masuala hayo.
Awali, baada ya kuwaapisha makamishna hao, Rais Kikwete, alisema ana imani nao kwa kuwa wana ujuzi wa kutosha kuhusu masuala ya utumishi wa umma, hivyo hakutakuwa na malalamiko, licha ya ugumu wa kazi hiyo.
Thursday, 12 March 2015
Watumishi wa umma watakiwa kuzingatia miiko na maadili
08:14
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru